Wakenya wangali wanapiga kura licha ya muda wa
mwisho wa shughuli hiyo kutimia.Upigaji kura ulianza asubuhi na mapema
baadhi ya wagombea wakiwa katika vituo vya kupiga kura saa nane na saa
tisa usiku.
Baadhi ya vituo vya kupigia kura vimefunga rasmi shughuli ya kupiga kura baada ya muda wa mwisho wa shughuli hiyo kutimia.
Milolongo mirefu ilishuhudiwa katika sehemu nyingi za nchi baadhi zikiwa hata karibu kilomita moja, ishara ya walivyojitokeza wakenya kwa shughuli hiyo ambayo ni ya kihistoria.
Kuna hofu kuwa huenda shughuli hiyo ikaendelea hadi usiku kwani milolongo bado ni mirefu sana.
Kwa hili kuna taarifa kuwa baadhi ya wagombea wanapinga swala la kuendelea na shughuli ya kupiga kura kwa hofu ya wizi wa kura.
Karani wa uchaguzi katika moja ya vituo vya kupigia kura mjini Nairobi
Katika sehemu mbali mbali kulikuwa na visa vya vurugu mfano mjini Mombasa ambako wanachama wa kundi la MRC waliwashambulia polisi waliokuwa wanashika doria na kuwaua wanne.Pia waliwaua raia kadhaa wasiokuwa na hatia.
Lengo la kundi hilo lilikuwa kuvuruga uchaguzi mjini Mombasa pwani ya Kenya.
Kundi hilo limekuwa likitaka uhuru wa jimbo hilo kwa madai kuwa wametengwa na serikali.
Magombea wa urais Raila Odinga aliwataka wananchi kustahimiliana pamoja na kuwapongeza kwa kupiga kura kwa utulivu.
Akina mama waliokuwa na watoto waliruhusiwa kupiga kura bila kupanga foleni
Nae Uhuru Kenyatta alisikitishwa na matukio ya Mombasa na kuwambia wakenya kuwa watulivu pia.
kwa mujibu wa idhaa ya kiswahili ya BBC, foleni mjini Nakuru zimeanza kupungua
Matokeo ya uchaguzi yanatarajiwa kutangazwa leo usiku ingawa tume ya uchaguzi inadai hadi siku saba ili kutoa matangazo ya matokeo ya kura za urais.